Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeelezea matumaini ya wakimbizi kurejea mashariki mwa DR Congo

UM umeelezea matumaini ya wakimbizi kurejea mashariki mwa DR Congo

Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa wanaozuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo wameelezea matumaini kwamba hali ya usalama itaimarika karibuni ili kuruhusu wakimbizi kurejea nyumbani mashariki mwa nchi hiyo na kuanza kilimo.

Mmoja wa maafisa hao Antonio Guterres ambaye ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR amesema wakati idadi ya watu wanaorejea na kuendesha shughuli zao katika eneo hilo inaongezeka, lengo la wakimbizi wote kurejea litafanikiwa tuu endapo usalama wa raia utakuwa ajenda inayopewa kipaumbele kitaifa na kimataifa.

Naye mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Josette Sheeran amesema hana mashaka kwamba endapo watapewa msaada unaohitajika na usalama wanaoulilia watu wa Mashariki mwa Congo watafurahi kurejea kwenye ardhi hiyo yenye rutba kujenga upya maisha yao.

Bi Sheeran amesema WFP ina mipango ya kuwasaidia kurejea nyumbani kwa amani wakimbizi hao kwa mradi maalumu utakaohusisha fedha, vocha na pia shirika hilo kununua bidhaa za kilimo zinazozalishwa na watu hao.