Majengo 50,000 yaliyoathirika na tetemeko Haiti huenda yakabomolewa

Majengo 50,000 yaliyoathirika na tetemeko Haiti huenda yakabomolewa

Wahandisi nchini Haiti wanaosaidiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za miradi UNOPS wamefanya tathimini ya majengo 200,000 ili kujua yalivyoharibika kutokana na tetemeko la ardhi la Januari 12.

Wahandisi hao wamekuwa wakiyalenga maeneo ambayo yameathirika zaidi na tetemeko hilo na kuingia kufanya ukaguzi wa kina kabla ya kuweka utepe wa rangi ya kijani, njano au nyekundu kutokana na kiwango cha uharibifu katika majengo hayo.

Majengo yaliyopewa kipaumbele ni shule na nyumba katika maeneo ambayo yamefurika watu wanaoishi kwenye mahema ya muda. Hadi sasa karibu nusu ya majengo yaliyokaguliwa yamewekwa utepe wa kijani ikimaanisha hayana uharibifu mkubwa wa kiufundi hivyo yanaweza kutumika bila hofu.

Zaidi ya robo ya majengo hayo yamewekwa utepe wa njano ukimaanisha kwamba kuna uharibifu ambao sio mkubwa sana na pia yanaweza kutumika baada ya kufanyiwa ukarabati, na asilimia 25 yamewekwa rangi nyekundu ikimaanisha yana uharibifu mkubwa na huenda yakabomolewa.