Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na IOC wanahimiza uchaguzi wa mfumo bora wa maisha

WHO na IOC wanahimiza uchaguzi wa mfumo bora wa maisha

Shirika la afya duniani WHO na kamati ya kimataifa ya olimpiki leo Jumatano wametia sahihi waraka mjini Lausanne Switzerland kuchagiza chaguo la mifumo wa maisha inayozingata afya.

Chaguo la mifumo hiyo ni pamoja na mazoezi ya viungo, michezo kwa wote, kutovuta sigara katika michezo ya olimpiki na kuzuia unene wa kupindukia utotoni. Chini ya makubaliano hayo WHO na IOC watafanya kazi pamoja katika ngazi ya taifa na kimataifa ili kupigia upatu uchaguzi wa shughuli na sera kuwasaidia watu kupunguza hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama magonjwa ya moyo, saratani na kisukari.

Mashirika hayo mawili pia yameafiki kuanzisha kikundi cha kufuatilia ambacho kitakutana angalabu mara moja kwa mwaka ili kufafanua zaidi, kuanzisha na kufuatilia mpango wa ushirikiano wa kimataifa na kutekeleza shughuli zenye lengo moja la kuokoa maisha.

Kwa mujibu wa WHO magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaua karibu watu milioni 35 kila mwaka ikiwa ni pamoja na milioni 9 ambao wako chini ya umri wa miaka 60. WHO imeonya kwamba vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vinaongezeka duniani kote na kwamba endapo hali hiyo itaendelea basi vifo vitaongezeka hadi kufikia milioni 41.2 ifikapo 2015.