Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO imeonya kuwa mlipuko wa polio Angola unaweza kusambaa

WHO imeonya kuwa mlipuko wa polio Angola unaweza kusambaa

Shirika la afya duniani WHO limeonya kuwa kuna hatari kubwa ya mlipuko wa polio wa hivi karibuni nchini Angola kusambaa katika nchi jirani na limetoa wito wa kuhakikisha kwamba watoto wanapewa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Takribani visa 15 vya polio type 1 vimearifiwa nchini Angola tangu mwanzoni mwa mwaka huu na WHO inasema dalili zinaonyesha kuwa ugonjwa huo unasambaa. Visa vyote ambavyo vimearifiwa vimetokea ama katika mji mkuu Luanda au majimbo mengine matano ya Bje, Bengo, Huambo, Lunda Kaskazini na Lunda Kusini ambayo awali yalitangazwa kuutokomeza ugonjwa huo.

Aina hiyo ya polio pia imebainika katika jimbo la nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwanzoni mwa mwaka. WHO inasema chanjo ya polio inahitaji kuimarishwa kwani karbu asilimia 25 ya watoto hawakuchanjwa katika msimu wa kampeni miezi 18 iliyopita. Pia shirika hilo limezitaka nchi jirani kuwa makini ili kuweza kukabiliana kwa haraka endapo ugonjwa huo utatokea katika nchi zao. Imewataka wasafiri pia wanaoingia na kutoka Angola kuhakikisha wamepata chanjo.