Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF inaunga mkono kampeni dhidi ya surua nchini Zambia

UNICEF inaunga mkono kampeni dhidi ya surua nchini Zambia

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO wiki hii yanaisaidia serikali ya Zambia katika jitihada za kujaribu kuwapa chanjo ya surua watoto zaidi ya milioni 1.6.

Kampeni hiyo ya nchi nzima ilianza jana mjini Lusaka na itaendelea hadi Ijumaa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNICEF ambayo inasema watoa chanjo wanawalenga watoto wa umri wa miezi tisa hadi 47.

Takriban watu 78 wamekufa na wengine karibu 3000 kuarifiwa kukumbwa na ugonjwa huo katika mlipuko wa karibuni wa surua na mji mkuu Lusaka ndio ulioathirika zaidi.

Surua ni ugonjwa unaoambukiza na unasambaa kwa njia ya hewa kama kukohoa na kupiga chafya. Ugonjwa huo unaambatana na matatizo ya kupumua, kuhara na uvimbe wa ubongo.