Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viet Nam imewapa hadhi ya utaifa wakimbizi wa zamani wa Cambodia

Viet Nam imewapa hadhi ya utaifa wakimbizi wa zamani wa Cambodia

Viet Nam inafanya juhudi kumaliza hali ya kutokuwa na utaifa kwa wakimbizi wa zamani wa Cambodia zaidi ya 2,300 ambao wengi wao wameishi nchini humo tangu 1975.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeipongeza Viet Nam kwa juhudi za kuwapa hadhi wakimbizi ambao ni kumbukumbu ya utawala wa Pol Pot. Kwa mujibu wa UNHCR takriban wakimbizi 290 wa zamani ambao wanaishi kwa yaliyokuwa makambi ya UNHCR nje kidogo ya mji wa Ho Chi Min wamepewa hati za uraia katika hafla maalumu.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Adrian Edward kupewa uraia kwa wakimbizi hao ni kutokana na juhudi za miaka mitano za shirika hilo na serikali ya Viet Nam. Shirika hilo linatarajia kuwa wakimbizi wengine wa zamani wa Cambodia 2,070 pia watapewa hadhi ya uraia ifikapo mwishoni mwa mwaka ili kumaliza hali ya kutokuwa na utaifa kwa watu hao.