Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zinafanyika kujiandaa na msimu wa kimbunga nchini Haiti

Juhudi zinafanyika kujiandaa na msimu wa kimbunga nchini Haiti

Juhudi zimeimarishwa nchini Haiti ili kujiandaa na majira yanayoambatana na mvua kubwa na kimbunga.

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM linasema mwaka huu kimbunga kinatoa tishio kubwa kwa sababu watu milioni 1.5 ambao ni wakimbizi wa ndani wanaishi kwenye mahema na makazi ya muda. Shirika hilo linasema washirika wake wanajiandaa kwa hali ngumu , na miongoni mwa maandalizi wanayoyafanya ni vifaa vya dharura vya malazi kwa ajili ya familia 25,000 na kuongeza uwezo wao hadi kuweza kusaidia familia 130,000 ifikapo mwezi Septemba.

Kwa mujibu wa msemaji wa IOM Jean-Philippe Chauzy jumuiya ya kimataifa pia inaandaa mipango ya mawasiliano kuwatayarisha Wahaiti kwa hali mbaya ya hewa na kusambaza ujumbe huo kwa jamii.

Mfano mameneja wa makambi watatumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kabla ya kuanza kwa kimbunga ili kuhakikisha wanawaandaa wakaazi tayari kwa kuhamishwa kwa dharura.