Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi mwema wa UNICEF na mwanasoka bora Messi azuru Haiti

Balozi mwema wa UNICEF na mwanasoka bora Messi azuru Haiti

Msakata kandanda maarufu ambaye ni raia wa Argentina Lionel Messi ameziuru Haiti ili kujionea changamoto zinazowakabili watoto miezi sita baada ya tetemeko la ardhi.

Messi amezuru nchi hiyo katika jukumu lake kama balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika ziara yake ya siku moja mwishoni mwa wiki Messi ametembelea kambi ya Carrefur Aviation inayohifadhi Wahaiti 50,000 ambao walipoteza nyumba zao wakati wa tetemeko la Januari 12. Tetemeko hilo lilikatili maisha ya watu zaidi ya 200,000 na kuwaacha wengine milioni 1.3 bila makazi. Messi mwenye umri wa miaka 23 amekutana pia na na wanajeshi wa Argentina wanahudumu katika mpango wa Umoja wa Mataifa Haiti MINUSTAH kupata taarifa za ulinzi wa amani na kuendesha hospitali wakati wa tetemeko.

Messi ambaye anachezea timu ya FB Barcelona ya Uhispania mwaka jana alikuwa mchezaji bora wa dunia wa FIFA, mshindi wa tuzo ya Golden Ball kwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya.