Skip to main content

Mkuu wa mfuko wa maendeleo ya kilimo IFAD yuko ziarani Rwanda

Mkuu wa mfuko wa maendeleo ya kilimo IFAD yuko ziarani Rwanda

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha maendeleo vijijini yuko nchi Rwanda ili kuimarisha ushirikiano na nchi hiyo ya Afrika katika suala la kililo, ambalo ni muajiri wa asilimia 80 ya watu wan chi hiyo.

Kanayo F. Nwanze ambaye ni Rais wa mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD, akiwa nchini humo kwa ziara ya siku tatu, amekutana na Rais Paul Kagame na maafisa wengine wa serikali kutoka wizara ya fedha, kilimo na biashara.

Ujumbe huo wa IFAD pia utakutana na wanaume na wanawake wa vijijini wanaoshiriki miradi inayofadhiliwa na IFAD, ambayo lengo lake ni kuwawezesha watu hao masikini kulima na kuuza chakula ili kujiongezea kipato.

Kilimo ndio uti wa mgongo wa Rwanda kikichangia takribani asilimia 36 ya pato la taifa kwa mwaka 2001 hadi 2008. Leo bwana Nwaze anazuru wilaya ya Bugesera mashariki mwa Rwanda ambako anazindua kituo maalumu cha jamii ambacho kitahusika na kutoa huduma na msaada kwa wakulima. Tangu mwaka 1981 IFAD imesaidia miradi 13 Rwanda iliyogharimu karibu dola milioni 150 na kuzifaidi familia zaidi ya 373,200.