Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 75,000 bado hawana makazi Kyrgyzstan mwezi mmoja baada ya machafuko:UM

Watu 75,000 bado hawana makazi Kyrgyzstan mwezi mmoja baada ya machafuko:UM

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya wakimbizi leo amesema watu 75,000 bado hawana makazi nchini Kyrgystan mwezi mmoja baada ya machafuko.

Machafuko ya mwezi June yalikatili maisha ya watu wengi, kuwaacha bila makao watu 400,000 na wengine wengi kulazimika kukimbilia nchi jirani ya Uzbekistan kupata hifadhi.

Katika miji ya Kusini mwa Kyrgystan ya Osh na Jalalabad ambako kulikuwa kitovu cha machafuko hali imetulia kwa sasa, lakini msemaji wa UNHCR Melissa Flemming amewaambia wandishi wa habari mjini Geneva kwamba kuna idadi kubwa ya polisi katika vituo vya ukaguzi na katika miji yote miwili watu hawaruhusiwi kutembea hovyo usiku.

Ameongeza kuwa hivi sasa watu 75,000 ikiwa ni pamoja na wale wanaoogopa kurejea nyumbani au na wale ambao hawawezi kwa sababu nyumba zao zimebomolewa bado wanahitaji malazi. Amesema kupotea kwa kwa nyaraka muhimu ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, paspoti, na hati za kumiliki ardhi inasababisha hali kuwa ngumu zaidi.