UNHCR imelaani kwa Uganda kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi wa Rwanda
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeiomba serikali ya Uganda kutoendelea kuwarejesha nyumbani kwa nguvu wakimbizi wa Rwanda kama walivyofanya mapema wiki hii.
Katika taarifa yake mjini Geneva UNHCR imelaani kitendo hicho. Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Melissa Fleming Wanyarwanda 1700 katika makambi mawili ya Uganda walikusanywa na kulazimishwa kuingia kwenye malori na kisha kusafirishwa kwa nguvu hadi kwenye mpaka wa Rwanda. UNHCR imelaumu hatua hiyo na ukatili wa polisi.
(SAUTI YA MELISA FLEMING)
Fleming amesema anafahamu makubaliano baina ya nchi hizo mbili ya kuwarejesha wakimbizi waliokosa hifadhi, lakini UNHCR haikuarifiwa muda na jinsi shughuli hiyo itakavyotekelezwa. Wakimbizi waliorejeshwa walikuwa washikiliwa kwenye kituo cha muda ambako walilala kwenye maeneo ya wazi bila chakula au maji safi.