Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitengo cha kesi cha ICC kimeamuru kuachiliwa huru Thomas Lubanga Dyilo wa DR Congo

Kitengo cha kesi cha ICC kimeamuru kuachiliwa huru Thomas Lubanga Dyilo wa DR Congo

Kufuatia uamuzi wa tarehe 8 Julai mwaka huu kuhusu kesi ya waendesha mashitaka dhidi ya kiongozi wa kundi la waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Thomas Lubanga Dyilo, kitengo namba moja cha kesi cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, leo kimetoa amri ya kumuachia huru mshitakiwa Lubanga.

Kwa mujibu wa majaji, mshutumiwa hawezi kushikiliwa kwa madai ya kukisia wakitaja kwamba hapo baadaye kesi inaweza kufufuliwa.

Hata hivyo amri hiyo ya kuachiliwa haiwezi kutekelezwa mara moja. Akithibitisha hilo jaji Adrian Fulford amesema leo kwamba amri hii haiwezi kutekelezwa hadi muda wa siku tano wa rufaa umalizike. Ameongeza kuwa kama rufaa itakatwa ndani ya siku tano dhidi ya amri hii ya kuachiliwa bwana Lubanga, na kama ombi litatolewa la kusitisha utekelezaji wake, basi mshutumiwa hawezi kuondoka rumande hadi kitengo cha rufaa kitakapoamua kama amri ya kumwlia huru isitishwe ama la.

Kitengo cha kesi pia kimesema kwamba amri ya kumuachia mshutumiwa itatekelezwa tuu baada ya kuwepo na mipango maalumu ya kumuhamisha kwenda kwenye taifa ambalo liko tayari kumpokea.