Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan imewatimua wafanyakazi wawili wa shirika la IOM Darfur

Sudan imewatimua wafanyakazi wawili wa shirika la IOM Darfur

Serikali ya Sudan imeliarifu rasmi shirika la kimataifa la uhamiaji IOM kuwa limewatimuwa wafanyakazi wawili wa shirika hilo na wametakiwa kuondoka mara moja.

Wafanyakazi hao wawili wa kimataifa wanafanya kazi ya kulinda na kugawa misaada kwa wakimbizi wa ndani, wale wanaorejea nyumbani na wengine walioathirika na vita kwenye jimbo la Darfur. Hakuna sababu zozote zilizotolewa za kwa nini uamuzi huo umechukuliwa. IOM inasema imesikitishwa na uamuzi huo ambao utaathiri uwezo wake wa kazi za misaada Darfur. Miongoni mwa shughuli za IOM Darfur ni kusafirisha bidhaa zisizo chakula na msaada kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na NGO'S yanayotoa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani.

Wafanyakazi wa IOM Darfur ni pamoja na mratibu mmoja aliyeko Khartoum, wafanyakazi 12 wa kimataifa na wafanyakazi 70 wazawa ambapo wamegawanyika katika ofisi tatu za Nyala, El Fashir na El Geneina.