Skip to main content

Utafutaji wa amani ya Darfur Sudan umepata nguvu asema Gambari

Utafutaji wa amani ya Darfur Sudan umepata nguvu asema Gambari

Mkuu wa mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye jimbo la Darfur Sudan UNAMID amesema utafutaji amani kwenye jimbo hilo umepata nguvu na uko katika hatua nyeti.

Ibrahim Gambari akizungumza leo katika duru ya pili ya majadiliano ya kutafuta njia za kutatua mzozo wa Darfur mjini Doha Qatar, amezitaka pande zote kushiriki mchakato wa amani. Gambari amesema ninawatolea wito wote ambao hawajashiriki na hasa kundi la Justice and Equality Movement JEM linaloongozwa na Dr Khalili Ibrahim kujiunga na mchakato kwa ajili ya amani na utulivu.

Mkutano huo unajumuisha pia wawakilishi kutoka mashirika na jumuiya za kiraia. Gambari amekaribisha habari kwamba Abdul Wahid Nur kiongozi wa kundi la Sudan Libetarion Army na Movement (SLA/SLM) ameelezea uungaji mkono wa mazungumzo ya amani ya Doha.