Skip to main content

Balozi wa UNICEF kukutana na watoto walioathirika na vita Uganda

Balozi wa UNICEF kukutana na watoto walioathirika na vita Uganda

Mcheza filamu na mwanaharakati Mia Farrow leo anakwenda nchini Uganda kama balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, ili kukutana na watooto walioathirika na vita.

Katika ziara yake ya siku tatu , Farrow atazuru eneo ka Gulu Uganda Kaskazini ambako atazungumza na watoto waliwahi kushikiliwa mateka na kundi la waasi la Lord's Resistance Army LRA, ambalo linafahamika kwa kuwatumia watoto jeshini, kuwasumbua raia nchini Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Pia atatembelea Kotido katika jimbo la Kaskazini Mashariki la Karamoja ambako watoto wanakabiliwa na ghasia zinazoendelea kutokana na mivutano ya kijamii.

UNICEF inasema eneo la Kaskazini mwa Uganda limeshuhudia miongo kadhaa ya vita baina ya serikali na kundi la LRA, na lina umasikini mkubwa, utapia mlo, idadi kubwa ya vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na watoto wengi kutosoma. Na kabla hajaondoka Bi Farrow atahudhuria kongamano la kwanza la vijana wa Afrika hapo Julai 17 mjini Entebe ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano wa tume ya Umoja wa Afrika na serikali ya Uganda.