Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa haki za binadamu waitaka Italia kufuta mswada wa upelelezi

Wataalamu wa haki za binadamu waitaka Italia kufuta mswada wa upelelezi

Serikali ya Italia imetakiwa ama kuufuta au kuufanyia marekebisho mswada wa sheria ya upelelezi na kusikiliza kwa siri mazungumzo kwa ajili ya uchunguzi wa uhalifu.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza Frank La Rue ameonya kwamba endapo sheria hiyo itapitishwa katika mfumo wa sasa itaweza kukandamiza haki ya uhuru wa kujieleza nchini Italia.

Kwa mujibu wa mswada wa sasa yeyote ambaye hana kibali maalumu cha uandishi habari anaweza kuhukumiwa kwenda jela hadi miaka mine kwa kurekodi mawasiliano ya aina yoyote au mazungumzo bila ruhusa ya muhusika na kuzitangaza habari hizo. Amesema hukumu kama hiyo itakandamiza kabisa uhuru wa mtu kutafuta na kutoa habari chini ya mkataba wa kimataifa wa haki za kijamii na kisiasa ambao Italia imeuridhia.