Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliotekeleza shambulio la kigaidi Uganda wafikishwe kwenye mkono wa sheria:Ban

Waliotekeleza shambulio la kigaidi Uganda wafikishwe kwenye mkono wa sheria:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la mabomu mjini Kampala Uganda lililotokea jana usiku na kukatili maisha ya watu wengi.

Shambulio hilo lilitokea wakati mamia ya watu wakiangalia fainali za kombe la dunia katika maeneo ya wazi kupitia runinga. Watu 64 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Ban amesema anatumai wahusika wa kitendo hicho watakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria. Ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya waliopoteza maisha, wananchi na serikali ya Uganda na amewatakia nafuu ya haraka majeruhi wote.

Kwa mujibu wa polisi nchini Uganda kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al-Shabab kutoka nchi jirani ya Somalia linashukiwa kuhusika na shambulio hilo. Umoja wa Afrika umekiita kitendo hicho ni shambulio la kigaidi na umetaka kilaaniwe vikali.