Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC imesitisha kesi ya Thomas Lubanga mbabe wa kivita wa DR Congo

ICC imesitisha kesi ya Thomas Lubanga mbabe wa kivita wa DR Congo

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imesitisha kusikilizwa kwa kesi ya mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anayeshutumiwa kwa kuwafunza na kuwasajili watoto jeshini.

Mahakama inasema kesi ya Thomas Lubanga imesitishwa kwa sababu waendesha mashitaka wakekataa amri ya kutoa maelezo ya ushahidi wake. Lubanga ambaye alikuwa mwanzilishi na kiongozi wa kundi la Union of Congolese Patriots UPC la jimbo la Ituri mashariki mwa Congo anakabiliwa na makosa mawili ya uhalifu wa vita. Moja ni kuwafunza na kuwasajili watoto jeshini na kujiunga na kundi lake, na pili kuwatumia watoto hao kushiriki mapigano ya kati ya Septemba 2002 hadi Agost 2003.

Kesi ya Lubanga ilianza kusikilizwa mjini The Haugue Uholanzi makao makuu ya mahakama hiyo, Januari mwaka jana 2009. Mahakama inasema pia kusitishwa kwa kesi hiyo ni kutokana na kuona kwamba haki kwa mtuhumiwa wa kesi hiyo itakuwa vigumu kupatikana kutokana na kutotekelezwa amri ya mahakama. Imesisitiza kuwa amri zote za mahakama lazima ziheshimiwe ili mahakama hiyo iweze kutekeleza wajibu wake.