Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Namibia yapongezwa kwa kuondoa vikwazo vya usafiri kwa wenye HIV

Namibia yapongezwa kwa kuondoa vikwazo vya usafiri kwa wenye HIV

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS limepongeza uamuzi wa serikali ya Namibia wa kuondoa vikwazo vya usafiri kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV.

UNAIDS inasema pia nchi hiyo imeidhinisha sheria inayofuata viwango vya kimataifa vya afya dhidi ya watu wenye virusi. Mabadiliko hayo ambayo yameanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu yameondoa masharti pia kwa watu wanaoishi na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Shirika hilo linasema hadi sasa hakuna ushahidi kwamba vikwazo kama hivyo vinazuia maambukizi ya HIV au kulinda afya ya jamii.Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe amesema amefurahishwa na kuguswa sana na tangazo hilo la serikali ya Namibia. Ameongeza kuwa vikwazi vya usafiri kwa watu wenye HIV havina maana yoyote na vinakuwa kikwazo kwa juhudi za kimataifa za kukabiliana na ukimwi. Amesema UNAIDS inapigia upatu haki ya mtu kuwa na uhuru wa kusafiri bila kujali wana HIV au la.