Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upungufu wa fedha unaweza kuwakosesha elimu watoto milioni 32 Afrika

Upungufu wa fedha unaweza kuwakosesha elimu watoto milioni 32 Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa lililopewa jukumu la kuchagiza elimu kwa wote leo limeonya kwamba ukosefu wa msaada unahatarisha juhudi za elimu Afrika.

Shirika hilo la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO linasema nchi za Afrika upungufu wa fedha hizo unaweza kuhatarisha juhudi za kuwarejesha shuleni watoto wapatao milioni 32 ambo kwa sasa hawasomi.

UNESCO imetoa onyo hilo wakati viongozi wa barani Afrika wakijiandaa kwa mkutano wa elimu wa kombe la dunia siku ya jumapili ijayo, ambayo ndiyo siku ya mechi ya fainali ya kombe la dunia mjini Pretoria Afrika ya Kusini.

Mkutano huo wa elimu ulioandaliwa na Rais Jacob Zuma unaadhimisha juhudi zilizoongozwa na kampeni ya 1Goal na shirikisho la soka duniani FIFA, ya kusukuma matatizo ya elimu Afrika katika ajenda ya juu ya kimataifa.Matatizo ya elimu Afrika yanarudisha nyuma ukuaji wa uchumi, upunguzaji wa umasikini, na upigaji hatua katika masuala kama ya afya ya jamii.