Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda imemtunuku mkuu wa vikosi vya kulinda amani Sudan UNAMID

Rwanda imemtunuku mkuu wa vikosi vya kulinda amani Sudan UNAMID

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wa Afrika UNAMID Prosefesa Ibrahim Gambari ametunukiwa tuzo ya Umurinzi.

Umurinzi ni medali ya kampeni ya Rwanda dhidi ya mauaji ya kimbari . Na tuzo hiyo amepewa na serikali na watu wa Jamuhuri ya Rwanda kutokana na juhudi na huduma zake kwa utu wa mtu. Akimkabidhi tuzo hiyo Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema "kwa uwezo niliopewa nakukabidhi Profesa Ibrahimu Gambari Umurinzi, medali ya kampeni ya Rwanda dhidi ya mauaji ya kimbari".

Bwana Gambari aikabidhiwa tuzo hiyo katika hafla maalumu iliyofanyika mjini Kigali Rwanda Julai 4. Rais Kagame amempongeza Gambari kwa jukumu lake la kuelimisha juu ya tishio la mauaji ya kimbari kwa wafanyakazi wenzie kwenye baraza la usalama na kulikumbusha baraza kila wakati kuchukua hatua kuzuia uasi Rwanda.

Rais Kagame amesema kuwa pia Gambari anastahili sifa kwa juhudi zake za kuleta amani sehemu mbalimbali duniani ili kuhakikisha kilichotokea Rwanda hakitokei tena popote pale. Amesema mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbari Rwanda Gambari alin'gamua mapema Februari kwamba nchi hiyo inatumbukia pabaya na kuchagiza baraza la usalama kuchukua hatua.