Wataalamu wa kimataifa wadhibiti kemikali ya melamine kwenye chakula
Tume ya Umoja wa Mataifa inayoangalia viwango vya chakula Codex Almentarius imetoa viwango vipya vya melamine katika chakula.
Tume hiyo inasema kiwango cha kemikali ya melamine kinachoruhusiwa kwenye maziwa ya unga ya watoto ni milgram 1 katika kilo moja. Na kiwango kinachoruhisiwa katika vyakula vingine na vyakula vya wanyama ni milgramu 2.5 katika kilo moja.
Melamine ni kemikali inayotumika kwenye bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa viwandani ikiwa ni pamoja na katika utengenezaji wa plastiki zinazotumika katika vyombo na vifaa vya jikoni na rangi ya makopo ambayo mara nyingi hujikuta imechanganyika kwenye chakula na haileti madhara yoyote, lakini inakuwa sumu kama inakuwa katika kiwango kikubwa.
Mwenyekiti wa tume hiyo Martin Weijtens amesema kuanzisha kiwango cha juu cha kemikali hiyo kutazisaidia serikali kutofautisha baina ya kiwango kidogo cha melamine ambacho hakina madhara kwa afya na kikubwa ambacho kinaathari, hivyo zinaweza kuwalinda watu wake kiafya.
Ingawa viwango hivyo vipya havibanwi kisheria lakini vinatoa uwezo kwa nchi kukataa kuruhusu uingizaji wa bidhaa zenye kiwango kikubwa cha kemikali ya melamine. Tume hiyo pia imetoa uamuzi wa kuboresha hatua za usafi kwa usalama wa chakula, mboga mbichi na vyakula vya baharini.