Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio dhidi ya gari la Umoja wa Mataifa laua mfanyakazi mmoja

Shambulio dhidi ya gari la Umoja wa Mataifa laua mfanyakazi mmoja

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa gari lake limeshambuliwa kwa risasi asubuhi ya leo mjini Kabul Afghanistan na kusababisha kifo cha mfanyakazi wake mmoja.

Taarifa iliyotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa wa msaada kwa Afghanistan UNAMA inasema Umoja wa Mataifa unalaani vikali shambulio katika mazingira yoyote yale dhidi ya wafanyakazi wa umoja huo.

Imeongeza kuwa wote waliohusika na mauaji hayo lazima wafikishwe kwenye mkono wa sheria bila kuchelewa.

Wafanyakazi wawili raia wa Afghanistan walikuwa wanasafiri katika gari hilo wakati liliposhambuliwa wakati wa msongamano mkubwa wa magari mjini Kabul, mfanyakazi mwingine waliyekuwa naye hakuumia. Mazingira ya shambulio hilo bado hayajafahamika lakini UNAMA inasema timu ya usalama ya Umoja wa Mataifa inashirikiana na taasisi za usalama za Afghanistan katika uchunguzi. UM umetoa rambirambi kwa familia ya mfanyakazi aliyeuawa ambaye jina lake bado halijatajwa.