Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunywa na kuchagiza zao la chai kutasaidia usalama wa chakula:FAO

Kunywa na kuchagiza zao la chai kutasaidia usalama wa chakula:FAO

Umoja wa Mataifa umewataka watu katika nchi zinazozalisha chai kuongeza uzalishaji kwa kutambua umuhimu wa kilimo hicho kwa kuhakikisha usalama wa chakula.

Shirika la chakula na kilimo FAO linasema usafirishaji nje wa zao la chai mfano nchini Kenya pato lake linatosha kulipa gharama za kununua chakula chote kinachoingizwa nchini . Kenya ni mzalishaji wa pili mkubwa wa chai duniani ukiacha Uchina. Chai inaweza kuwa kitu muhimu katika kuchangia usalama wa chakula amesema Kaison Chang, wa mamlaka ya chai duniani ya FAO.

Katika ripoti mpya FAO inazichagiza nchi wazalishaji wa chai kupigia upatu kinywaji cha chai zaidi nyumbani na kutangaza faida zake kiafya nje ya nchi, huku wakionya juu ya ongezeko la uzalishaji wake ambao unaweza kuathiri bei ya zao hilo baadaye.

Watumiaji katika nchi zinazozalisha chai wanakunywa moja ya kumi ya kiasi cha wanachozalisha ikilinganishwa na watu wa nje wanaoagiza kinywaji hicho limesema shirika la FAO. Kwa mujibu wa FAo bei ya chai ilipanda kwa asilimia 13 mwaka jana na kuifanya bei ya zao hilo kufikia kiwango cha juu kabisa ,kutokana na baadhi ya nchi wazalishaji za Afrika ka Asia kukumbwa na ukame.