Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Rwanda wahofia kurejea nyumbani yasema UNHCR

Wakimbizi wa Rwanda wahofia kurejea nyumbani yasema UNHCR

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyotolewa nchini Uganda inasema wakimbizi wa Rwanda wanahofi kurejea nyumbani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo miaka 16 sasa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda maelfu ya Wanyarwanda waliokimbilia mauji hayo wana wasiwasi wa kurejea nyumbani. Ripoti hiyo inasema licha ya kuwashawishi wakimbizi hao wameendelea kusisitiza kubaki nchini Uganda.

UNHCR inasema wakimbizi wanaohofia kurejea nyumbani ni wa jamii ya Wahutu wanakotoka wanamgambo wanaoshutumiwa kutekeleza mauji ya kimbari ambapo wengi waliouawa ni Watutsi. Ripoti hii imetoka wakati ambapo shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights watch limeilalamikia serikali ya Rwanda kwa kuendelea kukandamiza upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.