Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umelaani shambulio lingine dhidi ya kituo cha michezo cha UNRWA

UM umelaani shambulio lingine dhidi ya kituo cha michezo cha UNRWA

Mkuu wa uperesheni za misaada wa Umoja wa Mataifa Gaza amelaani shambulio la leo asubuhi katika moja ya vituo vya michezo vinavyotumiwa na watoto katika eneo hilo.

Hili ni shambulio la pili katika kipindi cha mwezi mmoja. Kundi la watu 25 waliokuwa na silaha na kuvalia vinyago walishambulia na kuchoma moto kituo cha michezo kilichoko ufukweni eneo la Nuseirat ambacho kilikuwa kinatumika kuendesha michezo ya kiangazi inayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA.

Hakuna aliyeumia kwenye tukio hilo ambalo linafuatia lile la Mai 23. Mkurugenzi wa UNRWA John Ging amelielezea tukio hilo kwamba ni la waoga na la kuchefua, na kuongeza kuwa mafanikio ya UNRWA yamewakera ambao hawapendi kuona watoto wana furaha. Ameongeza kuwa shambulio hilo halitoifanya UNRWA kusitisha na shughuli zake ambao ni kubwa za kuwapa fursa watoto wa Gaza ambazo ni pamoja na michezo, kuogelea, kuchora, kuchonga na kuigiza.