Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa G20, UM unatilia shime malengo ya maendeleo ya milenia

Mkutano wa G20, UM unatilia shime malengo ya maendeleo ya milenia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kutengamaa kwa uchumi wa dunia kunategemea kukua kwa nchi zinazoendelea.

Hiyo ni sehemu ya ujumbe wake kwa viongozi wa nchi 20 zilizoendelea wanaokutana mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa G20. Ban amesema kuna haja ya kuimarisha mtazamo katika masuala matatu, ambazo ni kipaumbele, ari ya kisiasa na ushirikiano. Na kusema kazi ya kwanza ni kazi. Ban amesisitiza kuwa huu ni wakati wa kujikita katika kazi za heshma, sio tuu kwa mataifa tajiri lakini kila mahali. Hii inamaanisha ni kuwekeza katika kazi bora, fursa za kiuchumi kwa wanawake na msaada zaidi kwa wafanyakazi duniani na wakulima wadogowadogo.

Ameongeza kuwa uchumi hauwezi kutengamaa bila kwanza kutengamaa kwa ajira. La pili ni utashi wa kisiasa na amesema daima mafanikio huanzia nyumbani, na nchi zinazoendelea lazima ziwe msitari wa mbele katika mipango ya kitaifa ili kufikia malengo ya milenia.

Na kuhusu ushirikiano Katibu Mkuu amekwisha tangaza jopo la kuchagiza malengo ya milenia ambalo anasema litamsaidia kuchagiza utashi wa kisiasa na kuwahamasisha watu kuanzia ngazio za chini kufikia malengo hayo.