Mcheza tenis mashuhuri kuzuru miradi ya vijana ya UM Chernobl

Mcheza tenis mashuhuri kuzuru miradi ya vijana ya UM Chernobl

Mcheza tennis mashuhuri ambaye ni balozi mwema wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Maria Sharapova atasafiri kutoka Wimbledon ambako anashiriki mashindano hivi sasa hadi Belarus kuzuru eneo lililoathirika na zahma ya nyuklia ya Chernobyl mwaka 1986.

Bi Sharapova atakwenda kwenye jimbo la Gomel, ambako shirika lake la hisani limesaidia kufadhili miradi mbalimbali ya UNDP inayolenga kutoa fursa za kujiendeleaza kwa vijana na kuboresha jamii zao.  Balozi huyo ambaye ni raia wa Urusi atazuru kituo cha utamaduni ambacho watoto wanafanya kazi ya kurembesha mji na kujifunza kuhusu mazingira. Pia atatembelea kituo cha afya kinachotoa tiba ya mfadhaiko wa akili na huzuni ya moyo. Mbali ya hayo atakutana na wanafunzi wa chuo kikuu wanaofadhiliwa na shirika lake.

Sharapova mwenye umri wa miaka 23, ambaye wazazi wake walikimbia Gomel mwaka mmoja kabla hajazaliwa kwa sababu ya kuhofia mionzi baada ya tukio la nyuklia la Chernobyl anasema nia yake ni kuwasaidia watu ili waweze kujisaidia katika eneo hilo ambalo linamgusa moja kwa moja. Mfuko wa Sharapova kwa ushirikiano na UNDP,wanasaidia miradi saba ya vijana na programu ya kutoa ufadhili wa shule katika maeneo yaliyoathirika na nyuklia ya Chernoby ambayo ni Belarus, Russia na Ukraine.