Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama limevitaka vyama vyote Burundi kushiriki uchaguzi

Baraza la usalama limevitaka vyama vyote Burundi kushiriki uchaguzi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limevitaka vyama vyote vya kisiasa nchini Burundi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Baraza hilo limeviomba vyaka kushiriki uchaguzi wa bunge utakaofanyika mwezi ujao na kujitahidi kuhakikisha uchaguzi wa Jumatau ijayo wa Rais unafanyika kwa amani na utulivu. Wito huo umekuja wakati kuna taarifa kwamba upinzani unagomea uchaguzi huo wa Rais.

Katika taarifa ya baraza hilo imeipongeza Burundi pia kwa hatua iliyopiga katika mchakato wa amani na kuruhusu mijadala ya kidemokrasia. Baraza limewataka wadau wote wa uchaguzi Burundi kuheshimu matokeo ya uchaguzi wa bunge utakaofanyika Julai 23 na 28 mwaka huu na wa Urais ambao utakuwa Juni 28.

Hata hivyo Burundi kwenyewe kuna taarifa kwamba kiongozi wa chama cha upinzani cha FNL Agatho Rwasa hajulikani aliko tangu jana hali ambayo imeanza kuzusha wasiwasi. Hata hivyo chama chake kimesisitiza kuwa Rwasa yuko mapumzikoni na hana nia ya kurejea msituni. Kutoka Bujumbura mwandishi wetu Ramadhani Kibuga anaarifu.