Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yafungua mahakama kuhukumu kesi za washukiwa wa uharamia

Kenya yafungua mahakama kuhukumu kesi za washukiwa wa uharamia

Serikali ya Kenya imefungua mahakama maalumu itakayotumika kuendesha kesi za washukiwa wa uharamia.

Mahakama hiyo imefunguliwa katika gereza la Shimo la Tewa mjini Mombasa katika pwani ya Kenya.

Jumla ya washukiwa 106 wanazuiliwa katika gereza hilo wakisuburi kukamilishiwa kesi zao. Maharamia wengine 18 tayari wameshahukumiwa na wanatumikia vifungo vyao katika gereza la Shimo la Tewa.

Mahakama hiyo maalumu inagharamiwa na Umoja wa Mataifa hasa ofisi yake ya madawa na uhalifu.

Serikali kadhaa pia zinachangia ikiwemo Marekani, Ufaransa, Canada na Ujerumani. Tayari ofisi ya Umoja wa Mataifa imeipa serikali ya Kenya dola milioni tano katika kuendesha mahakama hiyo. Jamii ya kimataifa imeeleza kuwa na imani kubwa kw kufunguliwa kwa mahakama hiyo ,na inasema itasaidia kuendesha haraka kesi za uharamia na hivyo kukabiliana na uharamia unaoendelea katika bahari ya Hindi.