Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon ametangaza mashujaa wa kusaidia kutokomeza umasikini

Ban Ki-moon ametangaza mashujaa wa kusaidia kutokomeza umasikini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametangaza kwamba anaanzisha kundi la watu mashuhuri la kujaribu kuelimisha na kuchagiza dunia kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo 2015.

Ban amesema kundi hilo ni nguvu za pamoja za mashujaa kuutokomeza umasikini na limechaguliwa kufanya kazi ya kuelimisha kuhusu malengo ya milenia. Kundi hilo litakuwa na wenye viti wawili Rais wa Rwanda Paul Kagame na waziri mkuu wa Uhispania Jose Luiis Rodriguez Zapatero.  Kundi hilo linajukumu la kumsaidia Bwana Ban kujenga utashi wa kisiasa na kutia shime hatua za kimataifa katika malengo manane ya milenia kabla ya kufanyika kwa mkutano wa ngazi za juu mwezi septemba kuhusu malengo hayo .

Bwana Zapatero atafanya mkutano wa kwanza wa kuhamasisha wa kundi hilo mwezi ujao mjini Madrid.

Ban amesema wakati wa mkutano wa Septemba lazima tuwe na mipango thabiti ya kitaifa ya kutimiza malengo hayo. Kila mjumbe wa kundi hilo ameambiwa kushughulikia moja ya malengo hayo katika uhamasishaji. Wengine katika kundi hilo ni mshindi wa tuzo ya amani ya nobel kutoka Bangladesh Muhammad Yunus, mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya Wangari Maathai na rais wa zamani wa Chile Michelle Bachelet.

Wengine ni mfanyabiashara mashuhuri Bill Gates na Ted Turner, mshauri maalumu wa Katibu Mkuu katika malengo ya milenia Jeffrey Sachs, na mshauri maalumu wa Katibu Mkuu katika masuala ya malaria Ray Chambers. Mbali ya hao wapo pia mke wa kiongozi wa Qatar's Bi Sheikha Mozah Bint Nasser, mke wa Rais wa zamani wa Msumbiji bi Graça Machel, Rais wa zamani wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson na Philippe Douste-Blazy, mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya fedha na ubunifu kwa ajili ya maendeleo.