Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wanaorejea nyumbani Kyrgystan walisalimishwe:UNHCR

Wakimbizi wanaorejea nyumbani Kyrgystan walisalimishwe:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeiarifu serikali na vyombo vya habari juu ya ongezeko la watu wanaorejea nyumbani kusini mwa Kyrgyzstan.

Shirika hilo limesema wanaorejea ni wale walikimbilia nchi jirani ya Uzbekistan na wengine ni miongoni mwa makundi ya wakimbizi wa ndani. Shirika hilo linasema ingawa haliwezi kutaja idadi kamili ya wanaorejea lakini idadi ya watu huenda ikafika 30,000.

UNHCR imepongeza juhudi za nchi zote mbili kujaribu kupata suluhu ya mgogoro wa sasa na kushughulikia mahitaji ya wakimbizi wa ndani. Pia imekaribisha hatua ya wakimbizi hao kurejea nyumbani na kuruhusiwa kuingia tena kwenye mpaka wa Kyrygyzstan.  Lakini limesisitiza kurejea kuwe kwa mpango, kwa hiyari na katika hali ya usalama na heshma na limeomba wanaorejea waende mahali ambapo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaweza kuwafikia.