Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 2.8 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula Niger:FAO

Watu milioni 2.8 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula Niger:FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani FAO linaimarisha shughuli zake za msaada kwa wakulima na wafugaji nchini Niger kama sehemu ya kukabiliana na tishio la njaa kwenye ukanda wa Sahel.

Msaada huo utawanufaisha watu milioni 2.8 ambao wanakabiliwa na njaa kutokana na mvua za msimu kutonyesha na hivyo kusababisha tatizo kubwa la upungufu wa chakula. Mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Khardiata Lo Ndiaye amesema hali ni mbaya sana kuliko ya mwaka 2005 na msaada wa haraka unahitajika kwani hali ya sasa haijawahi kuonekana hapo kabla. Amesema wanahitaji fedha na wanazitaka sasa.

Kwa mujibu wa FAO watu milioni 10 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa na wengine milioni 7.1 tayari wanakabiliwa na njaa. FAO inagawa mbegu na mbolea kwa wakulima katika msimu huu wa kupanda, mradi unaofadhiliwa na serikali ya Ubelgiji, Uingereza, Muungano wa Ulaya na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF). Mradi huo unagharimu dola milioni 17.7.