Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya wasiwasi imeendelea kulighubika eneo la Kusini mwa Kyrgyzstan: ICRC

Hali ya wasiwasi imeendelea kulighubika eneo la Kusini mwa Kyrgyzstan: ICRC

Kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu ICRC imesema hali ya wasiwasi imeendelea kutanda Kusini mwa Krygyzstan kwa siku tatu zilizopita. ICRC inasema hofu imetawala na jana vitendo vya ghasia vimearifiwa usiku wa kuamkia leo katika eneo la Osh.

Mjini Geneva msemaji wa ICRC Christian Cardon amesema kitu cha muhimu hivi sasa ni msaada wa kibinadamu kwa maelfu ya watu waliotawanyishwa na machafuko hayo. Amesema watu wanpata hifadhi katika misikiti, mashambani, vijiji vya jirani na katika majengo ya serikali ambayo ni matupu tangu kuzuka machafuko wiki jana.

Cordon amesema ICRC imeweza kuwatembelea mahabusu 1000 na kuwapa msaada wa chakula, lakini amesema haijulikani ni katika mazingira gani watu hao wanashikiliwa. Serikali ya Uzbekistan imewaandikisha watu wazima 75,000 ambao wamevuka mpaka na kuingia nchini humo kupata usalama.