Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu waliosambaratishwa na machafuko ndani ya Kyrgyzstan wamefika 300,000

Watu waliosambaratishwa na machafuko ndani ya Kyrgyzstan wamefika 300,000

Idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Kyrgystan kufuatia machafuko ya wiki jana inaendelea kuongezeka. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, taarifa kutoka serikali ya nchi hiyo na mashirika yasiyo ya kiserikali inakadiriwa watu laki tatu sasa wamesambaratishwa na machafuko hayo.

UNHCR inasema kwamba wakati wengi kati ya wakimbizi hao wa ndani wanahifadhiwa na familia na jamii, pia inakadiriwa kwamba watu takribani 40,000 wanahitaji malazi.

Shirika hilo linasema serikali ya kyrgystan inajaribu kurejesha sheria na hali ya utulivu na imearifu kuwa watu 180 wameuawa na wengine 1,900 wamejeruhiwa. Hali katika mji wa Osh na vijiji vya jirani bado ni ya wasiwasi.