Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama limelaani vikali ufundishaji na utumiaji wa watoto katika vita

Baraza la Usalama limelaani vikali ufundishaji na utumiaji wa watoto katika vita

Baraza la usalama limerejea wito wa kulaani vikali kuwafunza, kuwatumia, kuwauwa, kuwabaka, na kuwanyanyasa kwa aina yoyote ile watoto wakati wa vita.

Baraza hili pia limeelezea haja yake ya kuchukua hatua kali dhidi ya wanaoendelea na vitendo hivyo vya kihalifu. Katika taarifa ya rais wa baraza hilo kufuatia siku nzima ya mkutano, baraza pia limelaani ukiukwaji wa aina yoyote ile wa kimataifa dhidi ya watoto katika maeneo ya migogoro. Na limezitaka pande zote zinazohusika na vitendo hivyo kuacha mara moja na kuchukua hatua za kuwalinda watoto. Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa juni ni Mexico:

"Baraza la Usalama limeelezea hofu yake juu ya ongezeko la idadi ya mashambulizi au vitisho vya mashambulizi yanayokiuka sheria za kimataifa dhidi ya shule na vituo vya elimu, walimu na wanafunzi, na hususan yanayowalenga watoto wa kike. Na kwa maana hii tunazitaka pande zote zinazoshiriki vita kuacha mara moja ukiukaji huu na kuzingatia sheria za kimataifa na ubinadamu".

Baraza pia limekaribisha hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza azimio la mwaka 2009 kujumuisha pande zinazohusika katika vita ambazo zinajihusisha na mauaji ,unyanyasaji, ubakaji, na ukatili dhidi ya watoto.