Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serry ametaka mtazamo mpya kwa Gaza baada ya shambulio flotilla

Serry ametaka mtazamo mpya kwa Gaza baada ya shambulio flotilla

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Robert Serry, ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kwamba yeye na Katibu Mkuu wanaunga mkono mtazamo tofauti kwa Gaza baada ya tukio la flotilla.

Amesema tukio la flotilla ni dalili nyingine kwamba sera zilizopo zimeshindwa. Ameongeza kuwa hali ya Gaza ni mbaya na Israel lazima iondowe vizuizi vyake dhidi ya Gaza. Raia takribani tisa waliuawa na wengine 30 kujeruhiwa wakati jeshi la Israel lilipovamia msafara wa boti sita zilizokuwa na misaada ya kibinadamu ya kuipeleka Gaza.

Bwana serry amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba tume huru iliyotangazwa na Israel jana jumatatu kuchunguza tukio hilo lazima iende sambamba na uchunguzi wa kimataifa unaotakiwa na baraza la usalama . Robert Serry ametangaza kwamba Umoja wa Mataifa umekubali kuchukua jukumu la kuhakikisha boti ya flotilla ilishambuliwa inafika kunakohitajika na msaada unagawanywa Gaza kama lilivyoomba baraza la usalama.