Skip to main content

Msaada wa muda mrefu ni lazima ili kunusuru watoto Somalia:UNICEF

Msaada wa muda mrefu ni lazima ili kunusuru watoto Somalia:UNICEF

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Somalia Rozanne Cholton amesema watoto nchini Somalia wanahitaji msaada wa ndani na wa kimataifa wa fedha na vifaa ili kuhakikisha wanakuwa na maisha bora.

Bi Rozanne ameyasema hayo katika hafla maalumu iliyoandaliwa kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika ambayo kila mwaka huwa ni tarehe 16 june. Na mwaka huu kauli mbiu ni "mipango na bajeti kwa watoto ni jukumu letu sote"

Kwa miongo miwili sasa Somalia imeshuhudia vita na matatizo kwa watoto na wanawake. Hakuna hata motto mmoja nchini humo kwa sasa ambaye ameishi au kujua mazingira ya amani. Somalia inahitaji msaada wa fedha na vifaa kuhakikisha huduma kama za afya, lishe, elimu, maji safi, usafi na mambo mengine ya kuokoa maisha yanawasilishwa kwa watoto kama sehemu ya kujikomboa, ujenzi mpya na mipango ya maendeleo.

Bi Chorlton amesema jamii, familia, wazazi, viongozi wa jamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, wahisani na mashirika ya kimataifa wanatakiwa kuwa na jukumu la pamoja na kuweka mbele maslahi ya watoto.Na jukumu hili la pamoja ni lazima lijikite katika masuala mbalimbali ya mipango na bajeti kwa faida ya watoto wa Somalia.