UNICEF kuwaonyesha bure vijana Rwanda na Zambia kombe la dunia

UNICEF kuwaonyesha bure vijana Rwanda na Zambia kombe la dunia

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeanzisha mradi maalumu utakaowasaidia vijana wengine kwa mara ya kwanza kuona mashindano ya kombe la dunia kupitia runinga.

Mradi huo wa majaribio unaolenga maeneo ya vijijini kabisa yasiyo hata na umeme na hutuma ya televisheni umefanikiwa kwa ushirikano pia wa mfuko wa radio ya watoto na washirika wengine wa kijamii. Wa kwanza kufaidika na mradi huo mwaka huu ni vijana wa vijiji vywa Rwanda na Zambia ambako runinga kubwa zinazotumia projekta zimewekwa katika wilaya ya Rubavu Rwanda na mji wa Mongu na kwenye kambi ya wakimbizi ya Mayukwayukwa nchini Zambia.

Mashindano hayo ya kombe la dunia yataanza kuonyeshwa kuanzia siku ya ufunguzi Juni 11 hadi Julai 11. Mbali ya kandana matangazo maalumu yaliyoandaliwa na UNICEF kuhusu elimu, afya na kuwalinda watoto yatatolewa. Mambo mengine yatakayoambatana nayo ni mapambano dhidi ya ukimwi na mashindano ya soka kwa vijana.