Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani mauaji ya mwanaharakati wa haki DRC, wataka uchunguzi ufanyike

UM walaani mauaji ya mwanaharakati wa haki DRC, wataka uchunguzi ufanyike

Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa wamelaani vikali mauaji ya mwanaharakati wa haki za binadamu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema ameshtushwa na mauaji hayo ya Floribert Chebeya Bahirize na kutoweka kwa dereva wake Fidele Bazana ambaye hadi sasa hajapatikana. Naye mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay leo ameelezea kushtushwa na huzuni kubwa kutokana na habari za kifo cha mpigania haki huyo mashuhuri mashuhuri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo .

Mwanaharakati huyo maiti yake ilikutwa ndani ya gari lake nje kidogo ya mji mkuu Kinshasa jana. Mashirika ya kupigania haki za binadamu nchini humo yaliarifu kutoweka kwake baada ya kuitwa kwenda kwenye makao makuu ya polisi siku moja kabla.

Bi Pillay amesema kwa miaka 20 Chebeya Bahize amenusurika vitisho vingi vya kuuawa, kukamatwa na kuteswa kutokana na kazi yake ya kutetea haki za binadamu. Alikuwa akiamini umuhimu wa haki za binadamu na hakuogopa kuzipigania kwa kila hali. Chebeya alikuwa rais wa shirika lisilo la kiserikali lililojulikana kama Sauti ya wasio na sauti (VSV) ambalo alilianzisha mwaka 1988 na pia alikuwa katibu mkuu wa mtandao wa haki za binadamu nchini Congo RENADHOC.

Kifo chake ni pigo kubwa kwa jumuiya ya haki za binadamu sio kwa Congo tuu bali duniani kote, amesema Pillay akiutaka uongozi wa nchi hiyo kufanya uchunguzi wa kina wa kifo hicho na kutowafumbia macho wahusika.