Leo Mai 31 ni siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku

Leo Mai 31 ni siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku

Shirika la afya duniani WHO linasema uvutaji wa sigara miongoni mwa wanawake unaongezeka duniani kote,wakati makampuni ya sigara yakiwalenmga wanawake katika kampeni zake za kutafuta masiko.

Wakati leo ikiadhimishwa siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani WHO inasema miongoni mwa watu milioni tano wanaokufa kila mwaka kutokana na athari za tumbaku milioni 1.5 ni wanawake. Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku huadhimishwa kila mwaka tarehe 31 Mai na mwaka huu WHO inawalenga wasichana na wanawake na kutoa wito wa juhudi zaidi za serikali kuwalinda kutokana na uvutaji wa sigara na kushiriki biashara ya kutangaza tumbaku.

Shirika hilo linasema makampuni ya tumbaku yanawalenga wanawake na wasichana katika juhudi za kuchukua nafasi ya wanaoacha kuvuta au wanaokufa mapema kutokana na maradhi yanayochangia na bidhaa za tumbaku. WHO imeongeza kuwa makampuni ya tumbaku yanawafanya wanawake waamini kuwa uvutaji sigara ni ishara ya kustaarabika na inawasaidia kupunguza unene. Shirika hilo linasema wanawake wanaovuta sigara wako katika hatari ya kutokuzaa, kuzaa kabla ya siku na ongezeko la kupata saratani ya kizazi.