Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aipongeza Malawi kwa mafanikio ya kukabiliana na umasikini na njaa

Ban aipongeza Malawi kwa mafanikio ya kukabiliana na umasikini na njaa

Malawi lazima ijulikane duniani kote kwa mafanikio yake ya kupambana na umasikini na njaa na kuongoza katika kampeni ya malengo ya milenia.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini Lilongwe Malawi baada ya kuhutubia bunge la nchi hiyo jana. Ban amesema tunaweza na tutafikia malengo ya milenia akielezea hamasa ya kufanya hivyo ameipata Malawi. Ameongeza kuwa huo ndio ujumbe atakaoubeba kwenye mkutano wa mataifa manane tajiri duniani G-8 watakaohudhuria mkutano wa malengo ya maendeleo ya milenia mwezi wa septemba.

Malengo ya milenia yanatoa wito wa kufikia kuwa na elimu ya msingi kwa kila mtoto duniani, usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake, kupunguza vifo vya watoto na kina mama wajawazito, kudhibiti ukimwi, malaria na magonjwa mengine, kulinda mazingira na kuwa na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo.