Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya amani yanawezekana Cyprus katika miezi ijayo:UM

Makubaliano ya amani yanawezekana Cyprus katika miezi ijayo:UM

Maafikiano ya amani katika miezi ijayo yanawezekana kwenye kisiwa cha Mediteranian kilichogawanyika cha Cyprus.

Mtazamo huo umeelezwa na Umoja wa Mataifa wakati viongozi wa Ugiriki upande wa Cyprus Dimitris Christofias na wa Uturuki upande wa Cyprus Dervis Eroglu walipoanza tena mazungumzo ya amani baada ya miezi miwili ya mapumziko kwa ajili ya uchaguzi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika taarifa yake iliyosomwa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Alexander Downer amesema jumuiya ya kimataifa imejidhatiti kuendelea kutoa msaada kwa mchakato huo unaoongozwa na Cyprus, na anaamini kuwa pande hizo mbili zitafikia muafaka katika miezi ijayo.

Ban ameongeza kuwa mchakato wa amani ni muhimu , akisisitiza kwamba mpira hivi sasa uko mikonini mwa pande hizo mbili na wasipoteze fursa hii kwani muda waenda mbio.

Cyprus imegawaika mapande tangu mwaka 1974 wakati Uturuki ilipovamia theluthi ya kaskazini ya kisiwa hicho kufuatia mapinduzi ya maafisa wa Ugiriki.