Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa uhifadhi wa samaki duniani umeanza leo kwenye UM

Mkutano wa uhifadhi wa samaki duniani umeanza leo kwenye UM

Mkutano wa siku tano kuhusu uhifadhi wa samaki duniani umeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York.

Mkutano huo unaanza huku kukiwa na onyo kwamba robo tatu ya idadi ya samaki wako katika hali mbaya na karibu kutoweka wakati mfumo wa maisha ya viumbe wa majini ukizidi kuzorota.

Mwenyekiti wa mkutano huo David Balton ambaye ni naibu waziri wa Marekani wa masuala ya bahari na uvuvi ametaja uvuvi wa kupindukia, athari za uvuvi kwenye mazingira ya majini na haja ya msaada zaidi kwa nchi zinazoendelea ni miongoni mwa ajenda za mkutano huo.

Mkutano huo pia unatathimini utekelezaji wa makubaliano ya 1995 ya Umoja wa Mataifa kuhusu akiba ya samaki,ambayo yalianzisha sheria ya muda mrefu ya uhifadhi wa samaki na matumizi mazuri ya biashara kwa samaki hasa wanaohama kutoka eneo moja kwenda jingine.