Dunia ichukue mtazamo mpya ili kuiokoa Somalia katika vita:Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa dunia kuchukua mtazamo mpya ili kusaidia kuleta amani nchini Somalia.
Ban ametoa wito huo kwenye mkutano wa kimataifa wa kuhusu Somalia nchi iliyoko kwenye pembe ya Afrika , na amesema kwa kushindwa kuchukua hatua sasa kuna hatari ya machafuko ya Somalia kuingia kwa jirani zake na kwengineko.
Mbali ya hayo amesisitiza ujenzi mpya wa nchi hiyo iliyosambaratishwa na vita kwa kuwashirikisha jamii ya wafanya biashara wa Kisomali walioko ndani na nje ya nchi.
Mkutano huo wa siku tatu uliofanyika Istanbul na kufadhiliwa na Umoja wa Mataifa na serikali ya Uturuki umekuwa ukitathimini siasa za Somalia, usalama, na mahitaji ya ujenzi mpya mwaka mmoja baada ya mkutano kama huo kufanyika Brussels.