Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM imezindua mpango wa kuboresha maisha ya wakimbizi wa ndani Haiti

IOM imezindua mpango wa kuboresha maisha ya wakimbizi wa ndani Haiti

Kumekuwa na juhudi mpya za kubaini na kutimiza mahitaji ya wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni mbili wanaoishi kwenye makambi nchini Haiti baada ya tetemeko la ardhi Januari 12 mwaka huu.

Shirika la kimataifa la wahamiaji IOM linasema katika wajibu wake kama shirika linaloongoza kwa misaada ya dharura nchini Haiti hasa kuratibu na kusimamia makambi limeanzisha mipango mipya ya usimamizi kwa kuunda tume inayofadhiliwa na kitengo cha misaada ya kibinadamu cha muungano wa Ulaya.

Kwa mujibu wa Jared Bloch msemaji wa IOM timu hiyo itashirikiana na uongozi wa maeneo na viongozi wa jamii kuimarisha upashaji habari baina ya waathirika na watoaji wa misaada. IOM inasema pia itashirikiana na waratifu wa masuala ya afya nchini humo ili kuhakikisha wanatoa msaada wa vyandarua vya mbu 50,000 ambayo vimeshawasili nchini Haiti kukabiliana na msimu wa mvua.