Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya askari wawili wa UNAMID Darfur

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya askari wawili wa UNAMID Darfur

Takribani saa tano unusu asubuhi msafara wa magari matatu ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na wa Afrika Darfur Sudan UNAMID iliowabeba wanajeshi wa Misri ulivamiwa.

Msafara huo uliokuwa na  wanajeshi 20 ulivamiwa bila onyo na kundi lisilojulikana karibu na kijiji cha Katila kilomita 85 kusini mwa Edd Al Fursan, Kusini mwa Darfur. Wavamizi hao walikimbia baada ya majibizano ya risasi na msafara huo. Wanajeshi wawili wa kulinda amani wameuawa na  watatu wengine kujeruhiwa katika tukio hilo. Majeruhi wamesafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya UNAMID iliyoko Nyala Kusini mwa Darfur.

Mwakilishi maalumu wa juhudi za kutafuta amani ya pamoja wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, Ibrahim Gabari amelaani kitendo hicho dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani lakini ameongezea kuwa UNAMID iko kidete katika juhudi zake za kuleta amani kwa wakaaji wa Darfur.

UNAMID imeomba serikali ya Sudan kuwatambua, kuwashika na kuwapeleka mahakamani wavamizi hao na kuwakumbusha wahusika wote kuwa kuwavamia wanajeshi wa kulinda amani ya Umoja wa Mataifa ni kosa la uhalifu wa kivita.