Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Goodluck Jonathan aapishwa kuwa Rais wa Nigeria kufuatia kifo cha Yar'Adua

Goodluck Jonathan aapishwa kuwa Rais wa Nigeria kufuatia kifo cha Yar'Adua

Rais Umaru Musa Yaradua wa Nigeria amefariki dunia jana Jumatano saa tatu na nusu usiku. Kiongozi huyo alikuwa akiugua kwa muda mrefu.

Yar'Adua amezikwa leo alasiri nyumbani kwake kwenye jimbo la Katsina. Makamu wa Rais Goodluck Jonathan ameapishwa rasmi kuwa Rais wan chi hiyo. Rais Yar'Adua aliapishwa kushika hatamu za uongozi mwezi Aprili 2007 na kuwa Rais wa 3 wa Nigeria. Katika taarifa yake kufuatia kifo hicho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ameshitushwa na kuhudhunishwa na kifo cha Yar'Adua na ameongeza kuwa atakumbukwa pamoja na mambo mengine kwa juhudi zake za kurejesha amani na utulivu katika jimbo la Niger Delta.

Ban ameongeza kuwa pia alikuwa ni kiongozi aliyejidhatiti kuendeleza utawala wa demokrasia na mabadiliko ya kanuni za uchaguzi. Ban ametoa pole kwa familia ya Yar'Adua na taifa zima la Nigeria kufuatia msiba huo mkubwa kwa taifa.