Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyakazi wa UM huenda aliuawa na vikosi vya usalama vya Afghanistan

Mfanyakazi wa UM huenda aliuawa na vikosi vya usalama vya Afghanistan

Ripoti Umoja wa Mataifa kuhusu shambulio la kigaidi la mwaka jana dhidi ya nyumba ya kulala wageni ya Umoja wa Mataifa mjini Kabul, Afghanistan inasema kuna uwezekano kwamba mfanyakazi wa UM aliuawa kimakosa na vikosi vya usalama vya Afghanistan akidhaniwa kuwa ni mwanamgambo.

Ripoti hiyo iliyotolewa na jopo la wajumbe wanne lililoundwa Disemba mwaka jana limeainisha tukio hilo la Oktoba 28 mwaka jana ambapo wanajeshi watatu wa afghanistan na wafanyakazi watano wa Umoja wa Mataifa waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Ripoti hiyo imeelezea hali ya taharuki iliyojitokeza kwenye nyumba ya kulala wageni ya Bakhtar , huku washambuliaji na vikosi vya usalama vya Afghanistan wote wakiwa wamevalia sare za polisi wa Afghanistan na risasi zilizokuwa zikirushwa katika eneo hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amesema kwamba mlinzi afisa Louis Maxwell aliuawa akiwalinda wafanyakazi wenzie wa Umoja wa Mataifa wengi wao wangali hai hadi sasa kwa sababu ya hatua yake ya ushujaa. Ameongeza kuwa ripoti haikuweza kutanabahi nani alifyatua risasi ambazo ziliwauwa wafanyakazi wengine watatu wa UM ingawa haifuti uwezekano kwamba huenda waliouawa kwa bahati mbaya.

Ripoti hiyo pia imeelezea kasoro kadhaa katika hatua za usalama za umoja wa Mataifa pamoja na uratibu baiana ya UM na washirika wake wa kimataifa pamoja na serikali ya afghanistan.

Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameagiza kwamba mkuu wa masuala ya ulinzi na usalama Gregory Starr atathimini matokeo ya usalama ya ripoti hiyo.