Askari wa kulinda amani wa UNAMID waliotekwa Darfur wameachiliwa huru

26 Aprili 2010

Umoja wa Mataifa umesema wanajeshi wanne wa kulinda amani waliotekwa kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan mapema mwezi huu leo wameachiliwa huru.

Askari hao wawili wanaume na wawili wanawake kutoka vikosi vya muungano vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID walitekwa tarehe 11 Aprili kwenye mji wa Nyala ikiwa ni katika wimbi la hivi karibuni la utekaji wa wafanyakazi wa kigeni unaofanywa na kundi la vijana wanaotaka kulipwa kikombozi.

Mkuu wa UNAMID Ibrahim Gambari katika taarifa yake baada ya kuachiliwa askari hao amesema tunashukuru kuwapata wenzetu tena. Siku hii isingefanikiwa bila ushirikiano wa serikali ya Sudan na viongozi wa utawala wa Darfur.

Msemaji wa kundi linalojiita Movement for the popular struggle tarehe 20 mwezi huu alisema wanawashikilia walinda amani hao na wamekubaliana na serikali kuwachia huru. Amesema kundi lao halikulipwa kikombozi cha dola 450,000 walichodai kulipwa awali.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter